Sunday, April 23, 2006

UJAMBAZI: MAPIGO YA MWISHO AU YA MWANZO!

Hapa Mwanza ni karibia juma moja sasa limepita sijasikia tukio la ujambazi la kutetemesha. Sio kwamba hakuna matukio, lah!. Matukio yapo lakini naongelea matukio yale ya kutisha.

Kwa maana hiyo sisiti kuwapa pole wenzangu wa Dar-es-Salaam kwa tukio la namna yake. Kwa kweli tukio hilo limekuwa la kutisha sana kwani juzi wafanyakazi wa Benki ya NMB hapa Mwanza walionesha hali ya huzuni sana na kwa muda walikuwa wamepigwa na butwaa hali wakiendelea kuongelea tukio hilo lililowakumba wenzao. Hata hivyo walifarijiana wenyewe na kumaliza mjadala na kuendelea kufanya kazi.

Binafsi nawapa pole sana wenzangu wa Dar. Dar ni kuzuri kila mtu anachacharika ili awe na maisha mazuri na ndiyo maana basi wengine wanaona njia ya mkato ya kuwafikisha huko ni kumwaga damu za wenzao. Lakini pia sio wa huko Dar tu ndiyo mnataka maisha mazuri kwani hata sisi tuliopo huku mikoani tunaugua kaugonjwa hakohako.

Ni hivi juzi juzi tu wananchi wa Musoma wilayani Bunda walikutwa na tukio la namna hiyohiyo. Majambazi yalivamia mgodi wa Buhemba na kupora dhahabu. Tukio hilo inasemekana lilisukwa na walinzi wenyewe, na ndiyo maana walinzi kadhaa wa Kampuni ya SECURICOR bado wameshikiliwa polisi kwa kile kinachoonekana ni kuendelea kwa upepelezi zaidi juu yao.

Nilibahatika kuongea na mlinzi mmoja wa SECURICOR hapa Mwanza, kwani hapa Mwanza ndiko walikochukuliwa wenzao wa kwenda kuziba nafasi za wenzao walioshikiliwa huko Bunda. Mlinzi huyo akanipa rai kuwa yeye haoni ubaya wowote iwapo ni kweli wenzake watakuwa wamehuska katika tukio hilo.

Haoni ubaya huo kwa sababu anadai wazungu wa SECURICOR wamekuwa wakilipwa pesa nyingi sana kwa mkataba wa kutoa huduma ya ulinzi pale mgodini na sehemu zinginezo. Kiasi ambacho SECURICOR wanalipwa ni shilingi za KTz 700,000/- [yaani kilo saba] wakati wao wanamlipa kila mlinzi mwenye cheo cha chini kabisa shilingi 62,500/- yaani hapo ukitoa utaona kuwa makaburu hao wanachukua shilingi 637,500/- kwa kila kichwa. Walinzi wengi wa Kampuni hiyo ni wenye cheo cha chini ; 'masupavaiza' ambao huwa na mishahara ya shilingi 156000/- ni watatu tu. Mkuu wa masupavaisa ambaye kwa huko Buhemba mpaka sasa yupo ndani hulipwa shilingi 179,000 kati ya hizo kilo 7 ambazo huwazalishia makaburu.

Kwa mfano huu, pamoja na kuwa sijui NMB wanalipwaje, utaona kuwa ni rahisi sana mtu anayeminywa katika kipato chake akabuni utaratibu mwingine wa kusaplumenti hicho kidogo apatacho ili aweze kusavaivu. Kuna sehemu nyingi sana wafanyakazi wanalipwa ujira mdogo sana ukilinganisha na jinsi wanavyozalisha.

Katika kusema hivyo simaanishi kuwa wafanyakazi wajihusishe tu na ujambazi. Maana yangu ni kuwa tatizo hili linapaswa liangaliwe kwa undani sana kwani hata kama zitakuwepo helkopta za kupambana na uporaji bado ujambazi hautakoma kama watu wanaminywa katika ujira. Ikumbukwe kuwa pamoja na Raisi kusisitiza maisha bora kwa kila Mtanzania sio yeye atatuletea hayo maisha bora yeye ni msemaji tu kwani sisi wenyewe ndiyo tunapaswa kujitengenezea hayo maisha bora.

Sasa nitajitengenezeaje hayo maisha bora wakati wewe unanilipa shilingi 50000/- kwa mwezi na haunipi hata muda wa kutosha kufanya mambo yangu mengine? Mi kila kukicha kiwandani kwako, usiku ndiyo nakuwa kwangu na wakati mwingine inanipasa nirudi nyumbani usiku sana!

Nahitimisha hoja yangu kwa kutoa ushauri kuwa kupigana vita na majambazi kusiangaliwe katika kuimarisha jeshi la polisi tu, bali pia tuangalie hata wahusika katika utunzaji wa mali ibika. Hawa ndiyo watoaji wazuri wa raketi ya uporaji. Na wengi wao wanafanya hivyo kwa ajili ya kulipwa ujira mdogo, ingawa wapo pia na walafi.

Taasisi za mapesa zikizingatia hilo basi natumaini tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uporaji na tutakuwa pia tunaelekea katika njia sahihi ya kufikia maisha bora kwa kila Mtanzania.
!!!!!!!!!!!!!!!!?????????

No comments: